STORY: FAKE HISTORY (Historia Batili)
WRITER: Jumaa Khatib Mdharuba (Jk)
+255 718 274 130
+255 756 274 130
EPISODE 10
★★★★★★★★★★★★★★★★★
“Sijui ni nini kimempata huyu baba Abdul jamanii..mmmh..” Aliwaza Hamida baada ya kukata ile simu ambayo ilikua inaonekana haina majibu. Kisha akamgeukia mwanae ambaye alikua na hamu kubwa ya kufahamiana na baba yake na kumwambia..“Babaako ni mtu wa mambo mengi sana, akiwa free atanitafuta na utaongea nae usijali mwanangu”. Akaweka nukta kubwa huku akiweka sawa ukosi wa shati la rangi mbili- nyeupe na nyekundu alilokuwa amevaa Abdul.
Abdul'rahiim, kama lilivyosomeka jina lake kamili, alionekana kuridhika na maelezo haya ya mama yake akaitia ‘sawa’ kisha akauliza swali ambalo lilimfanya mama yake ahamaki na kumfanya amuangalie mtoto yule mara mbili mbili..
Licha ya kuwa na umri wake mdogo wa miaka tisa lakini alikuwa na uwezo mkubwa sana wa kufikiri na akili..Hakuwa akikurupuka katika kuongea mambo, na vitu vingi aliongea kwa kufikiri akiishirikisha akili yake katika kila analotaka kulitamka. Kwa sababu hii, si wanafunzi wenzake tu, bali hata walimu wote shuleni walimpenda sana na kuwa nae kwa karibu mno, wakifuatilia maendeleo yake kwa ukaribu mno huku wakihakikisha kuwa anapata haswa kile kilichompeleka shuleni.
Ni mwaka wa tatu mfululizo Abdul akiwa anazawadia tuzo ya mwanafunzi mwenye nidhamu zaidi shuleni. Awapo shuleni, Abdul alikuwa kipenzi cha wote.
Mama yake alikuwa akimueka katika mazingira ya usafi na kumfanya muda wote aonekane mtanashati, kila anayemtazama alikua na hamu ya kumuangalia tena.
“Mama, hivi kwanini wewe na baba hamuishi pamoja? Nini kiliwafanya mkatengana?” Hili ndilo swali gumu ambalo Hamida alikuwa hapendi aje aulizwe na mwanae..Si tu kwa sababu hakupenda mwanae afahamu undani wa baba yake ni nani, bali pia hakutaka mwanae ajue kuwa yeye alikuwa mtoto wa nje ya ndoa licha ya kuwa amelelewa katika mazingira ya kinidhamu sana na msimamo mzuri wa kidini. Jambo la yeye kuwa mtoto wa nje ya ndoa asingelikubali kirahisi, na huenda angeathirika haswa kisaikolojia-jambo ambalo Hamida hakutaka litokee kwa kipindi hiki.
Mama yake Hamida, bi Nana Amiry ambaye ndio bibi yake Abdul kwa upande huu wa mama yake alikua akisikia mazungumzo haya yanayoendelea kati ya Mwanae na mjukuu wake machachari Abdul.
Hamida alikua ndiye mtoto pekee wa bi Nana, na tangu kufariki kwa mumewe, Nana amekua akifarijiwa na hawa watu wawili tu, mwanae Hamida na mjukuu wake Abdul. Walikuwa wakiishi maisha ya kawaida sana, Hamida akifanya biashara za kukopesha nguo ambazo alikuwa akizifuata Kariakooo jijini Dar Es Salaam na kuja nazo mkoani Tanga walikokuwa wakiishi na mama yake. Na nje ya nyumba yao palikuwa na duka dogo la vyakula ambalo mara nyingi bi Nana ndiye alikua muuzaji wa duka lile, likiwaingizia pesa kidogo ambayo iliwawezesha kuwasukuma kimaisha kwa kadri riziki inavyopatikana.
Khatib, alikuwa akisaidia sana kwa nafasi yake kipindi cha nyuma kabla hajahamia Morogoro na pia hajawa mtu maarufu kama alivyo sasa..
Hamida alikuwa akimpenda saana Khatib, na hata kufikia kuzaa nae mtoto, japo bi Nana hakuridhika na jambo hilo kwa wakati huo.
Baada ya maisha ya Khatib kubadilika na kuhamia Morogoro, Khatib alianza kuwa 'busy' kidogo na mawasiliano aliyokuwa nayo kwa Mama hyu wa mtoto wake yalipungua kiasi kikubwa..Saa zingine Hamida alikuwa akipiga simu inaita na hapokei, saa zingine sms zake hazijibiwi..ilimradi palikuwa na mabadiliko.
“Sikiliza mwanangu nikwambie, hiyo ndo kawaida ya PESA, pesa inambadilisha sana mtu, sasa hapo huyo yeye anaona kama wewe unataka umuombe hela au umlilie shida zako wakati mwanzo mlikuwa mnawasiliana vizuri tu..” aliongea bi Nana kumwambia mwanae Hamida na kuongeza..“Sasa mwanangu, sisi rizki yetu inatoka kwa Mungu, na si kwake yeye huyo baba Abdul, wewe cha kufanya kwa sasa usimtafute mpaka akutafute wewe, na nisije nikasikia unamwomba pesa, mtoto huyu tutamlea tu na atakua kwa kudra za Mwenyezi Mungu” hapo ndipo alipokomea bi Nana na kumfanya Hamida kutafakari kwa kina kisha akachukua uamuzi wa kubadili namba yake ya simu ili hata hapo atakapotafutwa na Khatib awe hapatikani kabisaa..
Na hiki ndicho kilichotokea kwa miaka yote saba iliyopita, na kwakua Khatib alikua 'busy' sana na shughuli zake, mara chache alizobahatika kupiga simu na kukuta haipatikani zikazidi kumnyong'onyeza na kumfanya asipige simu tena..!!
“Bado hujakua mwanangu, upo muda ambao nitakueleza mimi na baba yako tulikutana wapi, tukaishi vipi, mpaka tukafikia hatua ya kukuzaaa wewe,..kwa sasa bado kidogo mwanangu..umenielewa?” Ndo maelezo aliyotoa Hamida kwa mwanae baada ya lile swali. Abdul alikuwa mdadisi, lakini hakuwa na pupa, na alikuwa akimsikiliza sana mama yake kwa kila analomwambia, kwahiyo aliridhika na maelezo haya na akaitikia kwa kichwa akimaanisha sawa..
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Habari za kuharisha mfululizo kwa Kulwa Yassini zilipenya taratiiib katika vikundi vya watu waliokuwa wamekusanyika katika maeneo ya karibu na nyumba ya msiba.. Kila mtu alianza kuhoji ni nini hasa kimetokea, wengine wakaanza kukata tamaa na azma ya Kulwa ya kuupeleka mwili wa marehemu Sauda hospitali kufanyiwa uchunguzi. Hii ni kutokana na muda kuwa umeenda sana na ni yeye Kulwa pekee ndiye aliyekuwa analiratibu jambo hili. Muda wa zaidi ya dakika 17 sasa Kulwa alikua hachezi mbali na mlango ule ambao ulikuwa hata hausindikwi kwa wakati huu kwa ajili yake tu..apate urahisi wa kuingia na kuachia vitu bila wasiwasi😃.
Mwili wake ulishaanza kukosa nguvu, maana aliharisha mfululizo sana, hivyo alipoteza maji mengi kwa muda mfupi..
“Kwahiyo Ma Mkubwa vipi, turuhusu mwili uende msikitini au tumsubiri huyu bwana mkubwa?” Aliuliza bwana mmoja mwenye umri wa miaka ya kijana, aliyeonekana kujazia misuli yake barabara..
“Pelekeni mwili msikitini mkauswalie kisha mkazike, huyo mwacheni aendelee na kuharisha kwake, mtoto mdogo balaa tele, kutuona watu wote hapa wapuuzi maanake nini, Mungu si huyo keshamlani aharisha sasa..” Aliropoka maneno mazito Mama Sauda akionesha msimamo wake waziwazi kuwa hakubaliani na jambo la Kulwa kutaka kupeleka mwili wa Sauda kwa uchunguzi zaidi.
*******************************
“Nasikia Kulwa anaendesha sana, ni nini kimemkuta sijui..?” Alihoji mzee mmoja anayekadiriwa kufikia miaka hamsini, akiwa amekaa nje ya nyumba ya msiba kwenye jamvi liliokuwepo chini ya mti wa mjohoro..Alikuwa ameketi yeye na wazee wengine watatu kwenye jamvi lile.
Mzee mmoja alionekana kuguswa zaidi na habari ile, na kuuliza kwa shauku..
“Kulwa huyu mtoto wa mdogo wangu Muna ndo anayeharisha?” akimtaja mama wa marehemu Sauda kama Muna, jina lake la kwenye vitambulisho.
“Ndiye yeye huyo, ana zaidi ya dakika ishirini sasa, tangu atangaze kuupeleka mwili hosptal kwa uchunguzi zaidi na kuhara kukaanzia hapohapo😀” Alifunguka mzee yule kwa maelezo mazuri yaliyonyooka..
Baada ya maelezo haya mzee huyu muulizaji maswali ambaye ni kaka mkubwa wa Muna-mama wa marehem Sauda, au twaweza kumuita mjomba wa marehemu Sauda, Jina lake likiwa Jumanne Selemani, wengi wakimjua kama Mzee J4, alinyanyuka moja kwa moja mpaka uani mwa nyumba ile ya msiba, akamkuta Kulwa amejiinamia kwenye mnazi kitamli uliokuwa karibu na chooni huku ameshikilia tumbo lake, akionesha kuwa linamuuma kwani alikua analia kama mtoto mdogo.
Akamgusa begani na kumfanya astuke..
“Ndio mjomba” ndicho alichokisema Kulwa baada ya kugeuka na kumuona aliyemshika begani.
Mzee J4 alimuangalia sana Kulwa usoni, kisha akasikitika, halafu akapitisha mkono wake wa kulia katika uso wa Kulwa kisha akamwambia..
“Maiti imeshatoka, twende msikitini ukamswalie mdogo wako swala ya mwisho hii..hii vita ni nzito..HUIWEZI, wewe bado mchanga sana”
“Sasa Mjomba nitaendaje na hali hii naendesha kweli??” Alihoji bwana Kulwa ambaye hata sauti yake ilikua ya kichovu sana.
“Hapana, huharishi tena kwa sasa..”
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Watch Out Episode 11
Follow IG: sir_mdharubajk
©2015
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni