Jumatatu, 20 Julai 2015

HISTORIA BATILI O25

RIWAYA: HISTORIA BATILI (Fake History)
MTUNZI & MWANDISHI: JK
+255718274130
mdharuba@gmail.com

            EPISODE 025
              0⃣2⃣5⃣
★★★★★★★★★★★★★★★★
ILIPOISHIA....
Baada ya simu kukatwa, ndipo Khatib akagundua kuwa wenzake walishatangulia na amebaki peke yake, akawasha gari, akageuza na kuitoa kwenye maegesho ya Hotel na kuelekea msibani.
Wakati yupo barabarani akiendesha kwa kasi, kwa mbaalii akaanza kukumbuka maneno ya mama yake kuwa Mzee J4 alipaswa kushughulikiwa mapema.

SASA ENDELEA....
“Haloo.. Habari?”
“Safi tu”
“Habari za siku?”
“Nzuri”
“Ok, nilitaka kukusalimia”
“Nashukuru”
“Ok siku njema”
“Asante”
Baada ya kuona akijibiwa 'shortcut' sana, Dr Iddi aliamua kukata simu bila hata kuongea kile alichokikusudia. Hamida alishaanza kusahau kuhusu Dr Iddi, yeye mawazo yake yote yalikua kwa Khatib tu muda wote. Baada ya simu hii akamfuata mama yake aliyekua chumbani kwake akipanga nguo zake kabatini baada ya kuzianua.
“Mama, Dr Iddi kanipigia simu, sielewi anachotaka”.
“Mmmh, leo hii ndio huelewi anachotaka Dr Iddi? Kakufanyaje kwani jamani?” Nana alishangaa sana jinsi mtazamo wa Hamida ulivyobadilika.
“Mimi sitaki kumkwaza Khatib jamani, yule ni mzazi mwenzangu.. Sasa yeye Dr Iddi si ni mtu na mkewe? Kwanini aanze kunipigia simu kunisalimia? Sisi ndio wagonjwa tunatakiwa tuwatafute wao hao madaktari, lakini nashangaa mimi, Dokta ndo anawapigia simu wagonjwa... Hivi hana wagonjwa wa kuwahudumia huko?” Hamida alifoka.
“Usiseme hivyo mwanangu, kwani salamu inatia mimba?”
“Hata kama salamu haitii mimba mama, yeye anachotafuta kwangu ni nini?”
“Hivi Hamida umesahau jinsi Dokta Iddi alivyosaidi kuokoa maisha ya mwanao Abdul? Umesahau kweli?”
“Mimi hata sikujua kinachoendelea kuhusu Abdul siku ile, nyinyi ndio mlikuja kunambia kuwa eti sijui bila Dokta Iddi mtoto sijui angekufa sijui utumbo gani huko..”. Hamida aliongea na mama yake katika hali ambayo ilionyesha kuwa hapendezwi hata kidogo na jambo la Dokta Iddi.
“Mmh makubwa haya jamani, huyu Khatib kwakweli, sijui kakupa nini wewe mwanangu”.
“Mama, unavyotaka kuniaminisha kuwa mimi nilikosea kuzaa na Khatib ni jambo lisilokuwa zuri..na halina tija, yule ndio babaake Abdul, vyovyote vile iwavyo”.
“Sawa mwanangu, nimekuelewa mummy”. Nana aliona ni busara kufunga mjadala huu, maana huenda ukawa mrefu na kufikia pabaya.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Lesangwa alifanya kazi kubwa sana na yenye mafanikio kwa upande wa Khatib na mamaake. Pesa aliyokuwa analipwa Lesangwa ilimtosha kufanya matumizi yake ya kila siku pasipo kuwa na shaka wala wasiwasi wowote na maisha. Alipewa pesa nyingi!!. Hizi zilimfanya awe mtumwa wa Mama Mdharuba ili asije akarubuniwa hata siku moja na kufanya mambo kinyume.
Mbali na pesa hizo, lakini pia alikuwa akisikilizwa sana katika shida zake zingine, tofauti na nje kabisa ya malipo ya kazi alizokuwa akizifanya.
Mtoto wake wa pekee aliyezaa na mke aliyenaye alisoma katika shule nzuri sana na ada akiwa analipa Mama Mdharuba. Hata gari analotembelea Lesangwa ilikua ni zawadi aliyopewa na Mama Mdharuba baada ya kumfanya kupata kiwanja kilichokuwa kinauzwa kwa shughuli za kibiashara licha ya kupambana na matajiri wakubwa zaidi waliokua na dau kubwa kumzidi. Yeye alifanikiwa kukipata kwa bei rahisi tena kwa haraka kupitia Lesangwa.
Lesangwa alikua na mchango mkubwa sana katika maisha aliyochagua kuishi Mama Mdharuba. Alimuheshimu mno, hii ni kutokana na kuwa hakuwahi kushindwa kazi yoyote kati ya zile alizotakiwa kuzifanya.
Kwa upande wake Lesangwa yeye hakuwa na namna nyingine zaidi ya kuifanya kazi aliyokuwa anaambiwa kwa wakati, na vilevile alitoa ushauri kuhusu mambo yao kwa kadri mambo yalivyokuwa yakienda.
Jambo la Khatib kutofanya vile alivyokuwa anashauriwa na mamaake kwa ushauri alioutoa yeye Lesangwa, alishang'amua kuwa tayari kuna tatizo kubwa linakuja mbele yao.
Tatizo hili ambalo sababu kubwa ni Mzee J4, lingeleta taswira mbaya na kumuharibia sifa Lesangwa. Alishaona nini haswa Mzee J4 yalikua makusudio yake, na hatma ya mambo yatakavyokuwa endapo Mzee J4 ataachwa aendelee kama alivyo. Alimfahamu vizuri Mzee J4, na alijua nini kinampa kiburi. Ingawa kwa misingi na mipaka ya kazi yake, alikuwa hafanyi chochote mpaka aamrishwe kufanya hivyo na mabosi wake. Na hili ndilo sharti la wataalamu wote. Kufanya jambo bila kumwambia haliwezi kumuongezea yeye 'credit' kwani unaweza kuamini kuwa mambo hayo yametokea tu kwa bahati wakati si kweli. Kumwambia kisha akafanya na yakatokea, ndiko kunampandisha yeye na kuonekana anaweza mambo, hii inamsaidia kwa maslahi yake ya baadae.
Hivyo, Lesangwa alisubiri amri ya 'kudeal' na Mzee J4, lakini amri hii ilionekana kuchelewa mno. Aliona jinsi gani Khatib alivyokosea kumpa nafasi Mzee J4, na jinsi gani angemtesa..
Mzee J4 kupitia jini wake Sayyeed alijitahidi sana kutafuta nani haswa aliyekuwa nyuma ya Khatib na mamaake katika upande huu wa ulimwengu usioonekana, lakini alifeli.!! Kufeli huku kulitokana na jinsi Lesangwa alivyokuwa amejidhatiti na kujiwekea ulinzi mzito wa kutoonekana kirahisi na maadui. Hali hii ilimpa tabu Mzee J4 kwani aliamini kwa namna moja ama nyingine ni LAZIMA watu hawa wangekuwa wanajihusisha tu na mambo haya. Lakini kwa nini Sayyeed anashindwa kung'amua?!..
Hii vita tayari Lesangwa alishaifahamu, lakini aliamua kusubiri 'outcome'.
*************************
“Haloo Mama, nipo msibani, Nira, yule aliyekua akisimamia pale yard amefariki. Kwahiyo ndio tupo katika taratibu za awali za maziko kabla ya kuupeleka mwili wa marehemu Mbeya kwa ajili ya mazishi”. Khatib alimpigia simu mamaake kumjulisha kinachoendelea.
“Sawa mwanangu, poleni sana na kila la kheri huko”.
“Ok, sawa mama Ahsante, ila kabla sijasahau naomba uongee na Sheikh Lesangwa umwambie ampunguze kasi Mzee J4, ameshakuwa tatizo”.
“Mzee J4 ni tatizo tangu mwanzoni, mimi nilimuona, sema wewe mwanangu saa zingine unakuwa mbishi kama shipa, sasa hapo yameshakutokea puani ndo unanambia nimtafute Lesangwa, wewe si uliamua kumkumbatia?”. Mama Mdharuba aliamua kumshambulia mwanawe baada ya kuelezwa kuhusu Mzee J4.
“Mama, niko msibani kama nilivyokwambia, kwahiyo nadhani huu ni wakati wa utekelezaji zaidi kuliko lawama. Naomba weka pembeni lawama kwa sasa, tu'solve' hili kwanza halafu uta'resume' lawama zako baadae.”. Khatib aliongea sentensi za kibabe katika hali ya ustaarabu.
“Sawa, ngoja nifanye hivyo, nitakutafuta baadae..”. Mama Mdharuba aliaga na kukata simu ili moja kwa moja amtafute Lesangwa.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Hisham ndiye mtu pekee aliyekuwa pale msibani na huzuni kuliko watu wote. Marehemu huyu kwenye kichwa cha Hisham alionekana ni mtu anaeenda kuyavuruga kabisa maisha ya Hisham.
Mlolongo wa mambo yote yatakavyoenda kitovu chake ni Nira.
Nira ndiye mtu aliyemwambukiza Regina Ukimwi, mwanamke aliyempenda na kuishi nae kwa miaka mingi. Kupitia Ukimwi huu ambao Nira ameupandikiza mwilini mwa Regina, umesababisha Regina atoroke. Kutoroka kwa Regina kunampa uhusiano mbovu na swahiba wake Khatib, na huenda pengine akaamua kumporomosha au kumuua kabisa kwa kushindwa kumuua Regina. Hili litapelekea maisha yake kuvurugika kabisa.
Mara nyingi Hisham amejikuta akizinduliwa kutoka katika dimbwi la mawazo wakati watu wakiwa katika mipango ya maziko ya Nira. Na hii ilichangiwa zaidi na sentensi ya Khatib mara tu baada ya kufika pale msibani, kwani alimuita Hisham na kumnong'oneza “Tutaongea baadae kuhusu jambo letu, hapa tuangalie msiba kwanza.. Ila jambo la Regina kutoroka HALIVUMILIKI”.
Neno HALIVUMILIKI lilikuwa likijirudia sana kichwani mwa Hisham na kumfanya azidi kuwa na mawazo muda wote.
HALIVUMILIKI ilikuwa haitafsiriki.
"Ni kwa kiasi gani hili jambo litakua halivumiliki kwa Khatib?" Ndilo swali lililokuwa kichwani mwa Hisham wakati wote. Alimfahamu vizuri Khatib kuwa ni mpole mbele ya macho ya watu tu-lakini sio uhalisia wake. Khatib ni muuaji, tena katili haswa ambaye kutoa roho ya mtu kwake lilikua jambo la kawaida sana.
“Bro, maiti hii lazima isafirishwe leo kwenda Mbeya, kwahiyo changamka ili tukamilishe utaratibu hapa haraka tuanze safari, naona una mawazo sana ndugu yangu, sijui tatizo ni nini?!” Haroun alivunja ukimya huku akiwa amemshika mkono Hisham aliyekuwa ameegemea nguzo ya turubai lililokuwa msibani hapo akimtaka atoe ushirikiano.
“Kazi niliyopangiwa na boss nimeikamilisha mapema tu kaka, labda wewe unataka nifanye nini?”. Hisham alimkodolea macho Haroun.
“Ok, sawa lakini unaonekana hauko sawa kaka, tatizo ni nini?” Haroun aliuliza
“Niko poa Haroun, kawaida tu.. Nahisi kama kijihoma kinaninyemelea”. Aliamua kudanganya.
“Ok, pole sana, maana nakuona umenyongea sana”.
“Ahsante sana bro”.

Baada ya mipango yote kukamilka, safari ya kuelekea Mbeya ikaanza mara moja, Khatib hakutaka kabisa waucheleweshe mwili ule kwa ajili ya mazishi. Pia alitaka ndugu zake Nira wapate kupata muda wa kutosha kuuaga mwili wa ndugu yao kabla ya kuuzika. Hivyo safari ya kwenda Mbeya ikaanza jioni ile ya saa 11. Hisham, Khatib na Haroun kila mmoja akiwa katika gari yake peke yake. Fred alikuwa katika Canter ndogo ambayo ndiyo ilibeba mwili wa marehemu. Huku ndugu na jamaa wengine wakiwa katika usafiri wao binafsi na wengine wakiwa katika 'Coaster mayai' mbili ambazo Khatib alizikodi. Gari ya Khatib ikitangulia mbele kwani ni yeye pekee ndiye alikuwa akipajua nyumbani kwa kina Nira. Ikafuatia gari yenye maiti, kisha ikafuatia ya Hisham, na ya Haroun na gari zingine ndogo nne, zikifuatiwa na zile Coaster mbili, safari ikaendelea.
**************************
“Khatib,uko wapi mwanangu?” Neno la kwanza la Mama Mdharuba baada ya simu yake kupokelewa na Khatib licha ya kuita muda mrefu sana.
“Niko Mikumi, ndio tunaelekea Mbeya hivi kwa ajili ya kuuzika mwili wa Nira”. Khatib alimjibu.
“Lini mtarudi huko?” Mama Mdharuba aliuliza kwa shauku.
“Ni mpaka tuuzike huu mwili, nadhani baada ya siku tatu.. Leo ni jumatatu kwahyo nafikiri kwenye Ijumaa hivi ndo tutakuwa tunarudi huko”. Khatib alitoa majibu kwa makadirio licha ya kuwa hajafika huko msibani na kuona hali itakuaje.
“Duuh, sasa ni hivii...” Mama Mdharuba alionekana kushangaa ratiba hii ngumu kwake.
“Enheee..nambie mama” Khatib aliitikia kutaka kujua mama yake anataka kusema nini!!.
“Ndio nimetoka kuongea na Lesangwa hapa, yeye amenambia kuwa unatakiwa uonane na Mzee J4 Tanga kesho Jumanne kabla ya saa saba mchana, ndio siku nzuri ya kumpatia pekee, kinyume na hapo HAIWEZEKANI tena na atatuathiri sana..kwahiyo nakuomba ufanye juu chini kuhakikisha kuwa unaahirisha hiyo safari ili ufanye hili la msingi kwanza..” Mama Mdharuba aliweka nukta ndogo kusikiliza Khatib atasema nini.
“oooohpsss... Daaaah..yaani hapo tu ndo tunapogombana mimi na nyinyi, mambo yenu mnapanga muda kama vile mimi sina shughuli zingine za kufanya..!! Angalia sasa..!!”. Khatib alimtupia lawama mamaake.
“Mwanangu, hizi zote ni juhudi zangu kuhakikisha kuwa 'status' yako haishuki, Lesangwa mwenyewe nimefanya kumbembeleza tu kwa sababu mwanzo ulishaonyesha kudharau.. Kwahyo hiyari unayo mwenyewe, kama utaenda kumzika Nira au utaenda kulinda status yako..kazi kwako, viwili vinachagulika”.
★★★★★★★★★★★★★★★★★

”Kila mtu ana matatizo, na huenda matatizo yako wewe kwa sababu ya kukosa pesa ni madogo zaidi kuliko ya yule mwenye pesa... RIDHIKA..” Mdharuba JK.

Tukutane Episode 26.

Jiandae kusoma kitabu, siku ni chache zimebaki ili kitoke.

Maoni: mdharuba@gmail.com
+255718274130

Alhamisi, 16 Julai 2015

HISTORIA BATILI O24

RIWAYA: HISTORIA BATILI
MTUNZI: Mdharuba JK
+255718274130
+255654727266

           EPISODE O24
               2⃣4⃣
★★★★★★★★★★★★★★★
ILIPOISHIA..
“Sawa kaka nimekupata, wewe nipe huu usiku halafu utaona”. Hishan aliitikia huku mwili ukimtetemeka.
“Poa, ila nakukumbusha tu kuwa ukiua kwa bastola ujue jela itakuhusu, sitakuwa na msaada kwako”. Mr Khatib alimalizia na kukata simu.
SASA ENDELEA...
Pamoja na shinikizo hili la kumuua Regina, Hisham alianza kumfikiria Regina kwa upande wa pili kama ambavyo alikua akiishi naye kwa kipindi cha miaka zaidi ya saba!
Alipata tabu sana kimawazo. Regina ndiye alikua mwanamke pekee ambaye alimjua vizuri Hisham, alimfariji, alimshauri, alimvumilia, alikuwa nae bega kwa bega tangu kipindi ambacho hana kitu mpaka leo akiwa ana maisha mazuri sana.
Hisham alikumbuka pia mara ya kwanza kukutana na Regina, akiwa amelewa 'chakari', hajitambui.. Regina alimsaidia.
Kilichokua kinamsumbua Hisham ni kuona kuwa anamuua Regina kwa sababu moja tu ambayo ni kulinda maslahi yake yeye na Khatib, lakini hakuwa na ubaya wowote katika nafsi yake.
Regina alikuwa mtu muhimu sana kwake, lakini alimfikiria rafiki yake Khatib, ambaye akienda kinyume na matakwa yake angekosa ushirikiano naye, na pengine hata angemuua!! Kichwa kilianza kumuuma..
Wakati yuko katika dimbwi hili zito la mawazo, ujumbe mfupi uliingia katika simu yake, akafungua na kuanza kuusoma..
“ Kaka, najua kinachokusumbua mpaka sasa ni kufikiria wema aliokutendea huyo mwanamke hadi leo, lakini unasahau kuwa huyo tayari ni mwathirika, alikusaliti, na angekuambukiza UKIMWI, sasa sijui ni kipi haswa kinakufanya usite kumuondoa, fanya maamuzi sahihi, wewe ni Jemedari wangu mkuu na nakutegemea sana kaka”..
Ujumbe huu ulimpa Hisham nguvu mpya na kunyanyuka pale alipo moja kwa moja akaelekea chumbani kwake.
Alimkuta Regina bado hajalala, akiangaza huku na huko mle chumbani.
“Mke wangu, mbona unaonekana kuwa na mawazo sana? Tatizo kubwa ni nini? Mimi sina kinyongo na wewe, na hya yote nimeshayasamehe, mbona unaonekana unashindwa kulala?”
“Hisham, najisikia vibaya sana, naomba unifungulie mlango nitoke nje kule kwenye bustani nikapunge upepo”.
“Ukapunge upepo usiku huu?”
“Ndio mume wangu, yanipasa kufanya hivyo kwa jinsi ninavyojisikia”
“Ok, sawa.. Twende pamoja”.
Hisham akafungua milango ya nyumba ile na kutoka na Regina mpaka katika bustani nzuri ya nyumba ile, sehemu waliyoweka maalum kwa ajili ya kupumzikia. Walijengea kibanda kidogo cha makuti na mabenchi ya mbao na meza vilivyochongeshwa kwa umaridadi mkubwa sana. Hapa palipendeza sana.
“Pole sana mke wangu, matatizo ni sehemu ya maisha, usihuzunike sana”. Hisham alijitahidi kumliwaza mkewe ili kumuonyesha kuwa yuko pamoja nae katika hali yoyote ile iwayo.
Kwa Regina kulikuwa na wazo tofauti, hakumuani Hisham hata kidogo, hapa alimwingiza katika mtego huu ambao alikua anaomba Mungu uende sawa.
“Natamani nipate juisi ya bariidiii..nipoze koo mume wangu” Regina aliongea baada ya mazungumzo ya muda mfupi.
“Kwahiyo unataka kuniambia kuwa unanituma niende ndani nikakuchukulie juisi?” Hisham aliongea huku akitabasamu.
“Yaah, mume wangu, nani mwengine wa kumtuma zaidi yako?” Regina aliongea naye akionyesha tabasamu lake kwa mara ya kwanza tangu asubuhi.
Hii ilimfanya Hisham aone kuwa sasa anakaribia kumteka Regina. Akachomoka mbio kuelekea ndani kwenye friji na kuchukua juisi.
Kwa Regina huu ndio muda aliokuwa akiusubiri.
Kiasi cha pesa ambacho alichukua mle ndani wakati Hisham akiwa sebuleni na kushindilia kwenye nguo yake ya ndani na zingine kwenye sidiria, aliamini kitaweza kumfikisha aendako salama.
Zilipita dakika tatu tu Hisham akarudi pale alipokuwa amekaa na mkewe, ila alishangaa kwa kuwa Regina hakuwepo eneo lile. Akaangaza huku na huko, bado Regina hakuonekana, akaanza kuita huku akizunguka maeneo mbalimbali ya nyumba ile lakini bado hakufanikiwa kumuona Regina!!. Akalielekea geti la nyumba ile na kufungua na kutoka nje huku bado akiendelea kuita bila mafanikio.
★★★★★★★★★★★★★★★★
“Inakuaje mama Mdharuba anakua sababu ya kifo cha mamaako?” Sarah alimuuliza Walter kwa hamaki kubwa akiwa haamini anachokisikia kutoka mdomoni mwa Walter.
“Mamaangu aliwahi kushiriki biashara na mama Mdharuba, miaka ya nyuma enzi ambazo mimi nilikua mdogo sana, ni baba ndiye aliyenieleza stori hiyo”. Walter alianza kufunguka.
“Enzi hizo bado Mama Mdharuba hajakuwa vile alivyo sasa, yaani namaanisha kuwa mwanawe bado alikua hajapata pesa zile alizonazo sasa..”
“Walter, unataka kunambia kuwa Mr Khatib hakurithi mali za babaake kama tunavyojua?”
“Pole mno Sarah,  yeetoh wejungulukwe ni kivwiri kibaha, kila upande wa mwiri wako kiathi ambacho kikugera kija mwaaka wethidhona  handu weelekea,,,harika uhana bahati mbivi mno hamwe naiti wethina ikotha (Pole sana Sarah, umezungukwa na kivuli kikubwa kila upande wa mwili wako, kivuli hiki kinakufanya uone giza kabisa na kutojua unakoelekea, wewe ni katika watu wenye bahati mbaya sana ingawa huna kosa). Walter aliongea kwa kipare kuweka msisitizo juu ya anachokiongea.
“Walter unaongea kwa mafumbo sana, nashindwa kukuelewa mylv”.
“Stori iko hivii... khatib na mama yake walikuwa watu maskini sana huko nyuma, hizi habari kuwa amerithi mali si za kweli, ila yapo waliyoyafanya..ila mimi sitakuambia lolote maana ukimchunguza bata utashindwa kumla..
Mama yake alishirikiana na mama biashara flani kipindi hcho, na baada ya kuwa wanaelekea kupata mafanikio makubwa, mama Mdharuba alifanya njia zake za kishirikina kama kawaida yake ili amzuge mama apate kumdhulumu, Mama hakukubali, ndipo akaamua na yeye kupambana. Ila hakujua kuwa mpambano huu alikua na nafasi ndogo sana ya kushinda,, angejua hivyo, angeacha, kuliko kutuacha sisi wapweke tukiwa bado wadogo sana. Kwahiyo mimi nikisikia kuhusu Mama Mdharuba nakumbuka tu mama yangu alivyofariki,.. Ila Sarah, sipendi kuongelea hili jambo tena, kwahiyo nakuomba usiniulize hata swali moja baada ya maelezo haya”.
“Ok, sawa baby, nimekuelewa”. Sarah aliitikia kinyonge ingawa alitaka kufahamu zaidi, hapa mawazo juu ya Khatib yalishabadilika.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Sasa ni majira ya saa tatu asubuhi, Mr Khatib akiisubiri kwa hamu simu ya Hisham, hatimaye simu yake ikaita, ila tofauti na alivyotarajia, mpigaji alikua Fred..
“Haloo, Fred vipi? Kwema?”
“Hapana, sio kwema boss”
“Nini tatizo tena?”
“Nimepata taarifa kuwa Nira amefariki muda huu, kwahiyo nilitaka nikujulishe kuwa nitafunga ofisi ili tuweze kuhudhuria huko msibani ili tuone taratibu za mazishi zinaendaje..”
“Oooh, ok, kumbe Nira amefariki..sawa.. Nadhani tutakutana huko haina shida”
“Ok, sawa boss”.
Baada ya kukata simu hii alimpigia simu Hisham,
“Mume mwenzako amefariki bwana Hisham”. Ndivyo alivyoongea Khatib baada tu ya salamu.
“Nani tena?! Nira au?” Hisham aliuliza kana kwamba hajui kuwa Mr Khatib alimaanisha nani.
“Yaah, fanya twende msibani, maana najua kazi ya kumpoteza Regina imekushinda”.
“Kaka wee acha tu, yule mwanamke kanitoroka jana usiku bana..”. Hisham alilalama akiwa anaamini Khatib hajui kinachoendelea.
“Pole sana, nilipewa taarifa leo asubuhi kuwa alionekana akitumia usafiri wa lori kuelekea kwao, nikajua tayari amekutoroka huyo, hakuna namna nyingine hapo”. Mr Khatib aliongea maneno ya kweli yaliyoashiria kuwa alikua na mtandao mrefu sana na kumfanya Hisham ajione bwege kwa kutomdhibiti Regina pale kwake.
“Kwahiyo unataka kunambia unajua anapoelekea?”. Hisham aliuliza swali hili ili ikiwezekana aanze kumfuatilia Regina na kufuta uzembe ambao ameonekana anao.
“Njoo tukutane Euler Hotel hapa tumchukue na Haroun tuelekee msibani, tutayaongea huko”. Khatib alimjibu Hisham na kukata simu.
“Sawa boss” Hisham aliitikia lakini simu ilishakatwa.
Wakakutana Euler Hotel wakajadili jinsi gani wataonyesha kuguswa na msiba ule na waubebe kama wao.
Hilo lilikua jambo la msingi sana kwao kuweka sawa 'status' zao kwenye macho ya watu. Licha ya kuwa vitu vingi anavyomilikia Khatib havikujulikana, lakini yard yake ikijulikana na kila mtu, na kila mmoja alijua kuwa Nira ndiye alimuajiri kuwa mkurugenzi wa pale. Hivyo watu wote wangetegemea kumuona Khatib akishiriki kikamilifu kwenye msiba ule.
“Haroun wewe nakukabidhi sekta ya vinywaji pale, hakikisha kwenye msiba huu watu hawakaukiwi maji kabisa, kama na soda zitakuwepo pia itakua poa sana.. Hisham utanisaidia kunitengenezea mandhari nzuri ya watakaokuja msibani, hakikisha hakuna mtu anakosa kiti, halafu pia ushughulike na masuala ya usafiri ili tuupeleke huu mwili kwao Mbeya kwa ajili ya kuzikwa, mimi niachieni suala la chakula, nitalimaliza mwenyewe, na kama nitahitaji msaada wenu nitawaambia..”. Mr Khatib alimaliza kugawa majukumu na kuweka sawa kila kitu kabla hawajafika eneo la tukio. Kutangulia kwa Fred eneo lile kuliwapa nafasi ya kujipanga kwani Fred anaweza kutuliza presha ile ya msiba iliyopo pale huku wakisubiri vigogo hawa ili waweze kuendesha msiba vizuri.
“Ok, sawa boss hakuna shaka” Aliongea Haroun ambaye muda mrefu sana alikua kimya.
Wakatoka hotelini pale na kuelekea kwenye magari yao na kila mmoja akazama kwenye gari yake tayari kwa safari ya kuelekea ulipo msiba.
Baada tu ya kuchomeka ufunguo, Kabla hajawasha gari yake, Khatib alisikia simu yake iliyokua mfukoni iki'vibrate' na kutoa mlio kuashiria kuna sms imeingia. Akaitoa mfukoni, na kusoma sms ile ambayo ilionekana kutoka kwa Mzee J4, ilikua na neno moja tu "NIPIGIE". Kitendo hiki kilimfanya Khatib asijiulize maswali mengi, moja kwa moja akampigia Mzee J4 kumsikiliza anasemaje.
“Ndio Mzee, Habari ya leo?”
“Niko salama tu kijana wangu, pole sana kwa kumpoteza Jemedari wako muhimu bwana Nira”.
“Asante sana, nimeshapoa mzee..taarifa hizi umezipata tayari? Maana msiba umetokea muda sio mrefu, na sijaanza bado kusambaza taarifa”. Khatib aliuliza kwa hamaki kanakwamba amemsahau Mzee J4.
“Hilo sio la msingi kwa sasa, ila nataka nikupe pole zaidi kwa kushindwa kufanikisha mpango wako haramu wa kumshawishi Hisham kumuua mkewe-Regina”. Khatib aliishiwa nguvu ghafla, hakuwa na la kuongea zaidi ya kumuacha Mzee J4 aendelee.
“Nadhani umesahau kuwa uliniahidi utaachana na haya mauaji, bado unaendelea, nilikuambia usinikere, nahisi umesahau licha ya kuwa uliniahidi kuwa hutonikera. Bado unafikiria kuwa kuua ni njia sahihi zaidi kwako,, nakupa onyo kwa mara ya mwisho”. Mzee J4 alionekana kuchukizwa sana, na baada tu ya maneno haya alikata simu.
Baada ya simu kukatwa, ndipo Khatib akagundua kuwa wenzake walishatangulia na amebaki peke yake, akawasha gari, akageuza na kuitoa kwenye maegesho ya Hotel na kuelekea msibani.
Wakati yupo barabarani akiendesha kwa kasi, kwa mbaalii akaanza kukumbuka maneno ya mama yake kuwa Mzee J4 alipaswa kushughulikiwa mapema.
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Mzee J4, Mama Mdharuba, Hisham, Walter, Sarah... Kila mmoja anasababisha tatizo lake kwa mtu mmoja tu, Mr Khatib!! Pesa ina matatizo mengi sana.

Dont Miss Episode 25

Nimerudi kama ifuatavyo...

Maoni: mdharuba@gmail.com
+255718274130

Kitabu kinakuja, jiandae kununua..!!.