Alhamisi, 16 Julai 2015

HISTORIA BATILI O24

RIWAYA: HISTORIA BATILI
MTUNZI: Mdharuba JK
+255718274130
+255654727266

           EPISODE O24
               2⃣4⃣
★★★★★★★★★★★★★★★
ILIPOISHIA..
“Sawa kaka nimekupata, wewe nipe huu usiku halafu utaona”. Hishan aliitikia huku mwili ukimtetemeka.
“Poa, ila nakukumbusha tu kuwa ukiua kwa bastola ujue jela itakuhusu, sitakuwa na msaada kwako”. Mr Khatib alimalizia na kukata simu.
SASA ENDELEA...
Pamoja na shinikizo hili la kumuua Regina, Hisham alianza kumfikiria Regina kwa upande wa pili kama ambavyo alikua akiishi naye kwa kipindi cha miaka zaidi ya saba!
Alipata tabu sana kimawazo. Regina ndiye alikua mwanamke pekee ambaye alimjua vizuri Hisham, alimfariji, alimshauri, alimvumilia, alikuwa nae bega kwa bega tangu kipindi ambacho hana kitu mpaka leo akiwa ana maisha mazuri sana.
Hisham alikumbuka pia mara ya kwanza kukutana na Regina, akiwa amelewa 'chakari', hajitambui.. Regina alimsaidia.
Kilichokua kinamsumbua Hisham ni kuona kuwa anamuua Regina kwa sababu moja tu ambayo ni kulinda maslahi yake yeye na Khatib, lakini hakuwa na ubaya wowote katika nafsi yake.
Regina alikuwa mtu muhimu sana kwake, lakini alimfikiria rafiki yake Khatib, ambaye akienda kinyume na matakwa yake angekosa ushirikiano naye, na pengine hata angemuua!! Kichwa kilianza kumuuma..
Wakati yuko katika dimbwi hili zito la mawazo, ujumbe mfupi uliingia katika simu yake, akafungua na kuanza kuusoma..
“ Kaka, najua kinachokusumbua mpaka sasa ni kufikiria wema aliokutendea huyo mwanamke hadi leo, lakini unasahau kuwa huyo tayari ni mwathirika, alikusaliti, na angekuambukiza UKIMWI, sasa sijui ni kipi haswa kinakufanya usite kumuondoa, fanya maamuzi sahihi, wewe ni Jemedari wangu mkuu na nakutegemea sana kaka”..
Ujumbe huu ulimpa Hisham nguvu mpya na kunyanyuka pale alipo moja kwa moja akaelekea chumbani kwake.
Alimkuta Regina bado hajalala, akiangaza huku na huko mle chumbani.
“Mke wangu, mbona unaonekana kuwa na mawazo sana? Tatizo kubwa ni nini? Mimi sina kinyongo na wewe, na hya yote nimeshayasamehe, mbona unaonekana unashindwa kulala?”
“Hisham, najisikia vibaya sana, naomba unifungulie mlango nitoke nje kule kwenye bustani nikapunge upepo”.
“Ukapunge upepo usiku huu?”
“Ndio mume wangu, yanipasa kufanya hivyo kwa jinsi ninavyojisikia”
“Ok, sawa.. Twende pamoja”.
Hisham akafungua milango ya nyumba ile na kutoka na Regina mpaka katika bustani nzuri ya nyumba ile, sehemu waliyoweka maalum kwa ajili ya kupumzikia. Walijengea kibanda kidogo cha makuti na mabenchi ya mbao na meza vilivyochongeshwa kwa umaridadi mkubwa sana. Hapa palipendeza sana.
“Pole sana mke wangu, matatizo ni sehemu ya maisha, usihuzunike sana”. Hisham alijitahidi kumliwaza mkewe ili kumuonyesha kuwa yuko pamoja nae katika hali yoyote ile iwayo.
Kwa Regina kulikuwa na wazo tofauti, hakumuani Hisham hata kidogo, hapa alimwingiza katika mtego huu ambao alikua anaomba Mungu uende sawa.
“Natamani nipate juisi ya bariidiii..nipoze koo mume wangu” Regina aliongea baada ya mazungumzo ya muda mfupi.
“Kwahiyo unataka kuniambia kuwa unanituma niende ndani nikakuchukulie juisi?” Hisham aliongea huku akitabasamu.
“Yaah, mume wangu, nani mwengine wa kumtuma zaidi yako?” Regina aliongea naye akionyesha tabasamu lake kwa mara ya kwanza tangu asubuhi.
Hii ilimfanya Hisham aone kuwa sasa anakaribia kumteka Regina. Akachomoka mbio kuelekea ndani kwenye friji na kuchukua juisi.
Kwa Regina huu ndio muda aliokuwa akiusubiri.
Kiasi cha pesa ambacho alichukua mle ndani wakati Hisham akiwa sebuleni na kushindilia kwenye nguo yake ya ndani na zingine kwenye sidiria, aliamini kitaweza kumfikisha aendako salama.
Zilipita dakika tatu tu Hisham akarudi pale alipokuwa amekaa na mkewe, ila alishangaa kwa kuwa Regina hakuwepo eneo lile. Akaangaza huku na huko, bado Regina hakuonekana, akaanza kuita huku akizunguka maeneo mbalimbali ya nyumba ile lakini bado hakufanikiwa kumuona Regina!!. Akalielekea geti la nyumba ile na kufungua na kutoka nje huku bado akiendelea kuita bila mafanikio.
★★★★★★★★★★★★★★★★
“Inakuaje mama Mdharuba anakua sababu ya kifo cha mamaako?” Sarah alimuuliza Walter kwa hamaki kubwa akiwa haamini anachokisikia kutoka mdomoni mwa Walter.
“Mamaangu aliwahi kushiriki biashara na mama Mdharuba, miaka ya nyuma enzi ambazo mimi nilikua mdogo sana, ni baba ndiye aliyenieleza stori hiyo”. Walter alianza kufunguka.
“Enzi hizo bado Mama Mdharuba hajakuwa vile alivyo sasa, yaani namaanisha kuwa mwanawe bado alikua hajapata pesa zile alizonazo sasa..”
“Walter, unataka kunambia kuwa Mr Khatib hakurithi mali za babaake kama tunavyojua?”
“Pole mno Sarah,  yeetoh wejungulukwe ni kivwiri kibaha, kila upande wa mwiri wako kiathi ambacho kikugera kija mwaaka wethidhona  handu weelekea,,,harika uhana bahati mbivi mno hamwe naiti wethina ikotha (Pole sana Sarah, umezungukwa na kivuli kikubwa kila upande wa mwili wako, kivuli hiki kinakufanya uone giza kabisa na kutojua unakoelekea, wewe ni katika watu wenye bahati mbaya sana ingawa huna kosa). Walter aliongea kwa kipare kuweka msisitizo juu ya anachokiongea.
“Walter unaongea kwa mafumbo sana, nashindwa kukuelewa mylv”.
“Stori iko hivii... khatib na mama yake walikuwa watu maskini sana huko nyuma, hizi habari kuwa amerithi mali si za kweli, ila yapo waliyoyafanya..ila mimi sitakuambia lolote maana ukimchunguza bata utashindwa kumla..
Mama yake alishirikiana na mama biashara flani kipindi hcho, na baada ya kuwa wanaelekea kupata mafanikio makubwa, mama Mdharuba alifanya njia zake za kishirikina kama kawaida yake ili amzuge mama apate kumdhulumu, Mama hakukubali, ndipo akaamua na yeye kupambana. Ila hakujua kuwa mpambano huu alikua na nafasi ndogo sana ya kushinda,, angejua hivyo, angeacha, kuliko kutuacha sisi wapweke tukiwa bado wadogo sana. Kwahiyo mimi nikisikia kuhusu Mama Mdharuba nakumbuka tu mama yangu alivyofariki,.. Ila Sarah, sipendi kuongelea hili jambo tena, kwahiyo nakuomba usiniulize hata swali moja baada ya maelezo haya”.
“Ok, sawa baby, nimekuelewa”. Sarah aliitikia kinyonge ingawa alitaka kufahamu zaidi, hapa mawazo juu ya Khatib yalishabadilika.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Sasa ni majira ya saa tatu asubuhi, Mr Khatib akiisubiri kwa hamu simu ya Hisham, hatimaye simu yake ikaita, ila tofauti na alivyotarajia, mpigaji alikua Fred..
“Haloo, Fred vipi? Kwema?”
“Hapana, sio kwema boss”
“Nini tatizo tena?”
“Nimepata taarifa kuwa Nira amefariki muda huu, kwahiyo nilitaka nikujulishe kuwa nitafunga ofisi ili tuweze kuhudhuria huko msibani ili tuone taratibu za mazishi zinaendaje..”
“Oooh, ok, kumbe Nira amefariki..sawa.. Nadhani tutakutana huko haina shida”
“Ok, sawa boss”.
Baada ya kukata simu hii alimpigia simu Hisham,
“Mume mwenzako amefariki bwana Hisham”. Ndivyo alivyoongea Khatib baada tu ya salamu.
“Nani tena?! Nira au?” Hisham aliuliza kana kwamba hajui kuwa Mr Khatib alimaanisha nani.
“Yaah, fanya twende msibani, maana najua kazi ya kumpoteza Regina imekushinda”.
“Kaka wee acha tu, yule mwanamke kanitoroka jana usiku bana..”. Hisham alilalama akiwa anaamini Khatib hajui kinachoendelea.
“Pole sana, nilipewa taarifa leo asubuhi kuwa alionekana akitumia usafiri wa lori kuelekea kwao, nikajua tayari amekutoroka huyo, hakuna namna nyingine hapo”. Mr Khatib aliongea maneno ya kweli yaliyoashiria kuwa alikua na mtandao mrefu sana na kumfanya Hisham ajione bwege kwa kutomdhibiti Regina pale kwake.
“Kwahiyo unataka kunambia unajua anapoelekea?”. Hisham aliuliza swali hili ili ikiwezekana aanze kumfuatilia Regina na kufuta uzembe ambao ameonekana anao.
“Njoo tukutane Euler Hotel hapa tumchukue na Haroun tuelekee msibani, tutayaongea huko”. Khatib alimjibu Hisham na kukata simu.
“Sawa boss” Hisham aliitikia lakini simu ilishakatwa.
Wakakutana Euler Hotel wakajadili jinsi gani wataonyesha kuguswa na msiba ule na waubebe kama wao.
Hilo lilikua jambo la msingi sana kwao kuweka sawa 'status' zao kwenye macho ya watu. Licha ya kuwa vitu vingi anavyomilikia Khatib havikujulikana, lakini yard yake ikijulikana na kila mtu, na kila mmoja alijua kuwa Nira ndiye alimuajiri kuwa mkurugenzi wa pale. Hivyo watu wote wangetegemea kumuona Khatib akishiriki kikamilifu kwenye msiba ule.
“Haroun wewe nakukabidhi sekta ya vinywaji pale, hakikisha kwenye msiba huu watu hawakaukiwi maji kabisa, kama na soda zitakuwepo pia itakua poa sana.. Hisham utanisaidia kunitengenezea mandhari nzuri ya watakaokuja msibani, hakikisha hakuna mtu anakosa kiti, halafu pia ushughulike na masuala ya usafiri ili tuupeleke huu mwili kwao Mbeya kwa ajili ya kuzikwa, mimi niachieni suala la chakula, nitalimaliza mwenyewe, na kama nitahitaji msaada wenu nitawaambia..”. Mr Khatib alimaliza kugawa majukumu na kuweka sawa kila kitu kabla hawajafika eneo la tukio. Kutangulia kwa Fred eneo lile kuliwapa nafasi ya kujipanga kwani Fred anaweza kutuliza presha ile ya msiba iliyopo pale huku wakisubiri vigogo hawa ili waweze kuendesha msiba vizuri.
“Ok, sawa boss hakuna shaka” Aliongea Haroun ambaye muda mrefu sana alikua kimya.
Wakatoka hotelini pale na kuelekea kwenye magari yao na kila mmoja akazama kwenye gari yake tayari kwa safari ya kuelekea ulipo msiba.
Baada tu ya kuchomeka ufunguo, Kabla hajawasha gari yake, Khatib alisikia simu yake iliyokua mfukoni iki'vibrate' na kutoa mlio kuashiria kuna sms imeingia. Akaitoa mfukoni, na kusoma sms ile ambayo ilionekana kutoka kwa Mzee J4, ilikua na neno moja tu "NIPIGIE". Kitendo hiki kilimfanya Khatib asijiulize maswali mengi, moja kwa moja akampigia Mzee J4 kumsikiliza anasemaje.
“Ndio Mzee, Habari ya leo?”
“Niko salama tu kijana wangu, pole sana kwa kumpoteza Jemedari wako muhimu bwana Nira”.
“Asante sana, nimeshapoa mzee..taarifa hizi umezipata tayari? Maana msiba umetokea muda sio mrefu, na sijaanza bado kusambaza taarifa”. Khatib aliuliza kwa hamaki kanakwamba amemsahau Mzee J4.
“Hilo sio la msingi kwa sasa, ila nataka nikupe pole zaidi kwa kushindwa kufanikisha mpango wako haramu wa kumshawishi Hisham kumuua mkewe-Regina”. Khatib aliishiwa nguvu ghafla, hakuwa na la kuongea zaidi ya kumuacha Mzee J4 aendelee.
“Nadhani umesahau kuwa uliniahidi utaachana na haya mauaji, bado unaendelea, nilikuambia usinikere, nahisi umesahau licha ya kuwa uliniahidi kuwa hutonikera. Bado unafikiria kuwa kuua ni njia sahihi zaidi kwako,, nakupa onyo kwa mara ya mwisho”. Mzee J4 alionekana kuchukizwa sana, na baada tu ya maneno haya alikata simu.
Baada ya simu kukatwa, ndipo Khatib akagundua kuwa wenzake walishatangulia na amebaki peke yake, akawasha gari, akageuza na kuitoa kwenye maegesho ya Hotel na kuelekea msibani.
Wakati yupo barabarani akiendesha kwa kasi, kwa mbaalii akaanza kukumbuka maneno ya mama yake kuwa Mzee J4 alipaswa kushughulikiwa mapema.
★★★★★★★★★★★★★★★★★★★
Mzee J4, Mama Mdharuba, Hisham, Walter, Sarah... Kila mmoja anasababisha tatizo lake kwa mtu mmoja tu, Mr Khatib!! Pesa ina matatizo mengi sana.

Dont Miss Episode 25

Nimerudi kama ifuatavyo...

Maoni: mdharuba@gmail.com
+255718274130

Kitabu kinakuja, jiandae kununua..!!.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni