STORY: *HISTORIA BATILI*
MTUNZI: *Mdharuba, J.K.*
+255718274130
mdharuba@gmail.com
www.mdharubajk.blogspot.com
*EPISODE 029*
★★★★★★★★★★★★★★★★★★
ILIPOISHIA...
Sayyeed anamuua Sheikh Lesangwa bila hata kuagizwa na Mzee J4.
Upande wa pili nako Walter anampa mimba Sarah, shemeji yake Khatib, lakini anakataa wazo la Sarah la kutaka mimba hiyo itoke.
Nuro, Ahmed na Rukia wako katika kikao kizito kutaka kujadili hatma yao katika kazi wanayofanya, Nuro akionekana kuwa na wazo zuri.
Hamida naye anapigiwa simu na Dokta Idd kuhusu mgonjwa anayehisi anafahamiana nae.
Je, nini kinaendelea...
Fuatiliaa.....
“Dokta, naomba unipeleke nimjue huyo mgonjwa tafaadhali” Hamida alimwambia Dokta Idd huku akionyesha kuwa na wasiwasi mkubwa mara tu baada ya kufika pale hospitali na kuonana na Dokta Idd.
“Nifuate” Dokta Iddi alisema bila kuongeza neno lolote jingine.
Wakaongozana mpaka Wadi namba 4 ya hospitali ile, mlangoni paliandikwa *Ward 4-Men*. Wakaingia ndani Dokta Iddi akiwa mbele Hamida nyuma.
“Lahaulaaaa... Baba Abdul.. Jamaaniiii... Nini kimekupata Baba Abdul?” Hamida alihamaki mara tu baada ya kutupa jicho kushoto mwa wadi ile na kumtambua mgonjwa ambaye haswa Dokta Iddi ndiye alitaka aje amtambue.
“Kwa sasa mwache kwanza apumzike, maadamu umeshamtambua” Iddi alimshika mkono Hamida ambaye alikuwa ameinamia kwenye uso wa Khatib aliyekuwa hajitambui kwa wakati huu.
Wakaondoka pale wadini wakielekea katika ofisi ya Dokta Iddi.
“Majina ya huyu mgonjwa yalifanana kabisa na ya yule mwanao Abdul, nikahisi watakuwa na uhusiano, kumbe ni kweli” Dokta Iddi alianza kumuongelesha Hamida wakati akifungua mlango wa kuingia ofisini kwake.
“Ni kweli, yule ndio babaake Abdul”
“Oooh.. Oky, sawa.. Aliletwa hapa na Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mzee J4, akasema yeye ni msamaria mwema tu ameamua kumleta hapa hospitali. Na pia amenikabidhi funguo za gari alilomleta nalo akidai ni gari yake huyu mgonjwa” Dokta Iddi alitoa maelezo haya huku akifungua droo ya meza yake na kutoa funguo kisha akazitupia pale juu ya meza.
“Mmmh, mbona maelezo hayajanyooka hayo? Ni Mzee gani huyo Dokta jamani?..” Hamida alihitaji ufafanuzi zaidi juu ya hili, bado lilikuwa na mkanganyiko.
“Mimi sijawahi kumuona kabla ya leo”
“Ok, haya basi tusubiri mgonjwa apate fahamu huenda akatueleza kilichotokea.. Lakini vipi ukiangalia hali yake, anaweza akazinduka kweli?” Aliuliza kwa shauku, alishakuwa na wasiwasi mkubwa juu ya huyu mzazi mwenzie, na muda huu ndio muda ambao alihitaji kuwa karibu zaidi na Khatib baada ya kuonyesha nia ya dhati ya kutaka kuwa nae.
“Tumuombe Mungu” Ndio maneno pekee aliyoweza kuyasema Dokta Iddi kwa wakati huu.
★★★★★★★★★★★★★★★★
Baada ya Hisham, Haroun na Fred kuongoza msafara na kufanikiwa kufika Mbeya salama, hali ilikuwa tofauti na walivyoitarajia huko Mbeya. Wazazi wa Nira na wanaukoo wote waligoma kuupokea mwili wa marehemu Nira hadi hapo watakapomuona Khatib amekanyaga Mbeya. Hisham na Haroun walijitahidi kwa kadri ya uwezo wao kuwashawishi ndugu wa marehemu Nira lakini juhudi zao ziligonga mwamba.
“Wewe unajua huyo Khatib wakati anakuja hapa kwa mara ya kwanza alituambiaje?! Ni lazima aje yeye, hatuwezi kupokea maiti bila ya yeye kuwepo hapa” Alipigilia msumari wa mwisho Mzee mmoja aliyekuwa amevalia suruali nyeusi na koti kubwa jeusi huku ndani akivalia t-shirt nyeupe ambaye alijitambulisha kama Mzee Mwanachia.
Hisham ndiye aliyeonekana kuchanganyikiwa zaidi.. Akajaribu kupiga simu kwa Khatib, lakini haikupokelewa.
“Sasa tunafanyaje hapa kaka?” Hisham alimuuliza Haroun katika sintofahamu ile.
“Mimi sijui, maana nimejaribu kumpigia bosi hapokei”
“Tulishamjaribu mara zaidi ya ishirini tukiwa na Fred pale chini ya mti, hakupokea, sijui bosi ana tatizo gani kwakweli”. Alisisitiza Haroun ambaye aligundua kuwa Hisham hakuws akijua kuwa bosi wao hakuwa mwenye kupokea simu kwa muda mrefu sasa na si mara moja tu aliyomjaribu yeye.
“Hawa wazee watatufanya wajinga kaka, tugeuze tu na maiti yetu bana” Hisham aliongea kwa hasira. Haroun hakumjibu chochote alimwangalia kisha akatabasamu.
★★★★★★★★★★★★★★★★★
“Mwanao amefariki, yupo Mochwari ya hospitali ya Bombo jijini Tanga” Alisema Mzee J4 baada ya simu yake kupokelewa. Mama Khatib alipigwa na butwaa, hakuamini hiki anachokisikia. Akakata simu haraka haraka na kuamua kumpigia mwanawe, simu yake haikupokelewa. Akapiga zaidi ya mara tatu katika simu yake ya dharura pia haikupokelewa. Akaamua kumpigia Hisham.
“Mbona rafiki yako hapokei simu, kuna tatizo lolote?”
“Ni muda mrefu sasa tunashangaa hata sisi mama, sijui nini tatizo” Hisham alijibu na kumfanya Mama Khatib azidi kuchanganyikiwa. Akakata simu ile haraka ili ampigie Sheikh Lesangwa.
“Haloo.. Samahani Sheikh Lesangwa ameuawa kikatili sana hapa nyumbani kwake” Ilisikika sauti ya upande wa pili baada ya simu yake kupokelewa. Akahisi kuchoka, mawazo mengi sana yakamzonga.
Akafikiria kwa dakika kadhaa..hakujua cha kufanya. Akamfuata Hawa aliyekuwa chumbani kwake amejipumzisha na kumuamsha.
“Tuko katika matatizo makubwa mwanangu, mimi naelekea Tanga muda huu, kuwa makini mpaka nitakaporudi, pesa za matumizi utaangalia katika ile pochi yangu ya pink iliyopo kule chumbani kwangu” Hakupoteza muda mama Khatib baada ya kuhakikisha Hawa ameamka.
“Mama nieleze kwa undani basi ni.....?”
“Nitakueleza mwanangu ngoja niende huko Tanga kwanza”. Alimkatiza na kugeuza kisha akaelekea alipoegesha gari yake, safari ya kuelekea Tanga ikaanza.
★★★★★★★★★★★★★★★★★
“No, that was not my intention (Hapana, hilo halikuwa kusudio langu)” Alikuwa akijitetea Sarah wakati anatoa maelezo katika kituo cha polisi kikuu cha Jijini Vancouver, Canada. Afisa polisi aliyekuwa akifanya nae mahojiano alishindwa kuamini maelezo ya Sarah kuwa hakuua kwa kukusudia.
★★★★★★★★★★★★★★★★★
Nini kitaendelea...??!!
Endelea kufuatilia.. Episode 030
Kama hujasoma episode za nyuma kuanzia 1 hadi 29 ni 'simple'... Bofya hapa>>>www.mdharubajk.blogspot.com