Jumatano, 30 Machi 2016

HISTORIA BATILI 026

STORY: HISTORIA BATILI
MTUNZI : Mdharuba, J.K.

        EPISODE 26
**********************
Pamoja na kuwa wamefika Mikumi wakiwa wanaelekea Mbeya, Hisham bado alikuwa na mawazo mengi sana juu ya hatma yake na uswahiba wake na Khatib utakuaje. Aliwaza sana na akakosa majibu ya maswali yake.. Alikua akiendesha gari kuelekea msibani lakini hana furaha hata kidogo. Mawazo mengi sana yalimzonga. Alifikiria endapo Regina ataamua kwenda kutoa siri anazozijua kuhusu yeye Hisham, akianzia alipomkuta mpaka hapo alipomuacha.. Pia alifikiria kama Regina ataamua kueleza kwa undani uswahiba halisi uliopo kati yake na Khatib, alihisi kuchanganyikiwa.
Akachukua simu yake na kujaribu kumtafuta Regina, pasi na kutarajia simu ikaita.. Akasubiri kwa sekunde kadhaa kisha akiwa katika hali ya mshangao zaidi, simu ikapokelewa.
"Halooo.. "
"Haloo, Hisham vipi mume wangu?" Aliongea Regina kwa kujiamini, huku simu yake ikiwa imeunganishwa moja kwa moja kituo cha polisi. Regina aliona ni busara kuliripoti hili jambo polisi mapema ili ikitokea amepata tishio lolote linalohatarisha maisha yake basi polisi wawe na taarifa.
"Uko wapi Regina?" Aliuliza Hisham kwa sauti ya umakini.
"Nipo tu, nini unahitaji kutoka kwangu?" Aliuliza Regina naye kwa kujiamini.
"Kwa sasa nahitaji roho yako, hicho ndio muhimu sana kwangu" Alishapanic Hisham kama kawaida yake. Yaani kwake kuulizwa anataka nini lilishakuwa kosa. Akaamua kuropoka hivyo pasi na kujua kuwa simu yake ilikua ikirekodiwa.
★★★★★★★★★★★★★★
Baada ya kukata simu ya mamaake, Khatib aliamua kupunguza mwendo na kuwasha taa ya pembeni inayoashiria kuwa anataka kuliegesha gari. Hii ikalazimisha magari yote yaliyokuwa nyuma ya msafara kupunguza mwendo na kutaka kujua ni nini haswa kinaendelea huko mbele. Wengine walishahisi labda tembo wa mbuga hii ya wanyama ya Mikumi wameshaziba njia kwahiyo wanatakiwa kusubiri.
Khatib alilazimisha gari zote zilizopo katika msafara ule ziegeshwe huku akimtaka Fred (ambaye ndiye alikua na gari yenye maiti) awaite wote waliokuwa katika msafara ule, ana jambo muhimu la kuwaeleza. Fred akatekeleza.
"Ndugu zangu nimewakusanya hapa kuna dharura imejitokeza, sitaweza kuendelea na msafara huu kwa leo, natakiwa nirudi Morogoro kisha niende Tanga leoleo" Aliongea huku akizungushazungusha kichwa chake kujaribu kuangalia kila aliyepo pale. Hisham ndiye alikua wa kwanza kujibu.
"Boss, nini kimetokea hicho muhimu kuliko msiba wa swahiba wako na mfanyakazi wako bora kwa miaka mingi?!"
"Iko nje ya uwezo wangu hiyo Mr. Hisham" Khatib alimjibu kwa ufupi na kumfanya akose swali la kuendeleza. Kisha Haroun ambaye kawaida yake sio muongeaji, anaongea pale panapohitajika tu, alionekana kutaka kuongea kitu.
"Kaka, kitu unachotaka kukifanya kitaleta matatizo makubwa, fahamu kuwa ni wewe pekee ndiye unayefahamiana na ndugu zake huko kwao. Ni wewe pekee ndiye unayepajua kwao. Wewe ni mtu muhimu kuliko sisi sote. Sisi tunaweza tukarudi sote na ukaenda peke yako na bado kukawa hakujaharibika jambo, lakini kukosekana kwako wewe mmoja tu hata tukienda sote bado hatujafanya kitu. Kwahyo naomba ufikirie mara mbili uamuzi wako". Haruna ambaye ni mkubwa sana kwa Khatib alijitahidi kumnasihi mdogo wake huyu huku akiweka heshima ya 'uboss' palepale.
"Kinachonipeleka Tanga ni muhimu sana kuliko hiki, Nira ameshakufa, kuna maisha yetu wengine lazima yaendelee... Na hatujui tumepangiwa kuishi miaka mingapi, kwahiyo hatuwezi kushughulika zaidi na Nira ambaye tayari ni marehemu halafu tukasahau ya kwetu sisi wazima" Khatib aliongea kwa kujiamini na kusababisha kila mmoja akiinamisha kichwa chini akiwaza jambo lake.
Kikapita kitambo cha sekunde zaidi ya 30 watu wote wakiwa kimya. Khatib akaamua kutoa hitimisho.
"Mimi nawatakia safari njema, mkazike salama, naomba kwa sasa Fred ndiye awe kiongozi wa msafara.. Nitampa namba za wahusika huko Mbeya mtawasiliana nao. Ningefurahi kuona wote mkiendelea na msafara ili mkaniwakilishe vema". Akaweka nukta kubwa kisha akamvuta Fred pembeni kidogo wakaongea kiasi cha dakika tano, kisha akarudi kwenye gari lake na kugeuza na kuanza safari ya Tanga moja kwa moja.
★★★★★★★★★★★★★
"Vipi umefikia wapi mwanangu?" Aliuliza Mama Mdharuba baada ya kupiga simu kwa mwanawe huyu wa kiume.
"Ndo nipo njiani narudi, nimewaacha waendelee na msafara".
"Sawa, umefanya maamuzi ya busara sana, kwahiyo unaenda Tanga moja kwa moja??!"
"Ndio, au ulitaka nipite hapo Dar una maelekezo ya ziada?!"
"Hapana mwanangu, wewe kaendelee tu na mambo yako, tutajuzana baada ya wewe kufika".
"Sawa mama, hakuna shida".
"Ila Sheikh Lesangwa anaweza kukupigia maana alinamboa kuwa atahitaji kuongea na wewe kidogo katika mambo ambayo mimi amekataa kunieleza" Mama Mdharuba alionekana kama kukumbuka kitu.
"Sawa akinipigia nitamsikiliza" Khatib alimjibu mama yake.
Na baada ya kupita dakika tatu tu tangu akate simu ya mamaake, bado akiwa njiani kuelekea Moro kisha Tanga, Sheikh Lesangwa alipiga simu.
"Bwana Khatib mimi sina mengi ya kuongea, bali nakutaka utakapofika Tanga usikutane na yule mamaake Abdul, nenda kwa ajili ya Mzee J4 tu.
"Sawa Sheikh nimekuelewa.." Aliitikia Khatib na kukata simu.
Akaendesha gari hadi Morogoro mjini, akapitia nyumbani kwake mara moja. Hii ikiwa ni pamoja na kuibeba bastola yake ambayo kwenyr safari ya Mbeya aliamua kuiacha.
Akaanza safari ya kuelekea Tanga.
Akiwa ameshafika mizani ya Mikese ambapo ni nje kidogo ya mji wa Morogoro, simu yake ikaita. Baada ya kuiangalia, mpigaji alikuwa ni Mzee J4.. Akafikiria kidogo kabla ya kuamua kupokea. Akapokea..
"Karibu sana Tanga, nafurahi kuona unakuja kwa ajili yangu". Alisema Mzee J4 na kukata simu.

Nini kitaendelea??!!
Usikose Episode 27

Je, Ulikosa HISTORIA BATILI Episode 1 hadi Episode 25?!!

Bofya hapa...
👇🏿👇🏿👇🏿👇🏿👇🏿
http://mdharubajk.blogspot.co.ke/?m=1